Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amelitaka Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi pamoja na watendaji wake kuacha mara moja kulimbikiza kwa muda mrefu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kutokana na hoja hizo kukosa majibu.
Loata Sanare ametoa agizo hilo Mei 20 mwaka huu Wilayani Malinyi wakati wa kikao cha Baraza Maalum la Madiwani wakat wa kujadili taarifa na majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Loata Sanare amesema hoja za muda mrefu ambazo zinachelewa kupewa majibu ni dalili ya baadhi ya Watendaji wa Halmashauri kutotimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuwa kila hoja inamhusu mtendaji, hivyo haiingii akilini kukosekana kwa majibu hadi hoja hiyo kukosa majibu, na kwamba kikao hicho kiwe ndio mwisho wa kujadili hoja za muda mrefu.
“Kwa hiyo sitegemei kwa namna yoyote ile kuendelea kupata hoja ambazo zimepitwa na wakati, hoja za miaka ya nyuma mwaka huu tumefunga hazipo tena. Hoja hizi ambazo tumefunga kwa sababu hazina majibu hakikisheni zinapatiwa majibu”. Alisema Loata Sanare.
Aidha,amewataka watendaji wa Halmashauri hiyo kujiepusha kutotunza viambatisho katika utendaji wao hususan katika masuala ya manunuzi au kuingia mikataba mbalimbali badala yake wafuate utaratibu wa Serikali kwa kuwa baadhi ya hoja zilizopitwa na wakati zimekaa muda mrefu kwa sababu zimekosa viambatisho.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watendaji wa Halmashauri ya Malinyi kutofanya kazi kwa mazoea kwani hali hiyo inapelekea Halmashauri kudumaa na kutokuwa na mafanikio hivyo akawataka watendaji wote kuwa wabunifu katika utendaji wao.
Kuhusu madeni ya Halmashauri hiyo Mkuu wa Mkoa amelitaka baraza hilo la madiwani pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Malinyi Bi. Hawa Mpossi kulipa madeni wanayodaiwa kwa Taasisi na Wazabun ili kuepuka halmashauri kushtakiwa na au kuja kulipa fedha nyingi kuliko zinazodaiwa sasa.
Mwisho, Loata Sanare amerudia wito wake wa kuitaka idara ya Utumishi na Utawala kutenda haki katika kuwasikiliza watumishi wake na kuwapandisha watumishi wanaokaimu Ukuu wa Idara na vitengo badala ya watumishi hao kukaimu kwa muda mrefu hali inayosababisha kupunguza morali ya kazi .
Akitoa tahadhari juu ya agizo hilo la Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema ni kweli kuna taratibu na vigezo vinavyofuatwa katika kumpandisha mtumishi anayekaimu nafasi, hata hivyo amewataka viongozi wenye mamlaka kuwakaimisha watumishi wenye vigezo ili ukifika muda wa kuwaidhinisha kuwa Wakuu wa Idara waweze kuidhinishwa kwa urahisi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Malinyi Dkt. Haji Mponda akichangia hoja alizungumzia sekta ya miundo mbinu huku akiwatahadharisha Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) Mkoa wa Morogoro na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanya kazi zao kwa uadilifu kwani takwimu za nyuma zinaonesha kazi zao Katika Wilaya hiyo hazikamiliki kwa wakati hivyo kuleta manung’uniko kwa wananchi na kumwomba Mkuu wa Mkoa kulifuatilia jambo hilo.
Akifunga Kikao hicho maalum Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mheshimiwa Fadhili Liguguda alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kutekeleza na kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na kwamba kwa kuongoza kikao hicho maalum wameongeza uwezo wao na ujasiri mkubwa katika kuisimamia Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi hadi mwezi machi, 2020 ilikuwa na hoja 19 ambazo menejimenti ilitakiwa kuzifanyia kazi na tayari hoja 10 zimekwishafanyiwa kazi na zilizobaki hoja tisa zipo katika hatua mbalimbali ya kufanyiwa kazi.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.