Ilikuwa ni siku njema kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi pale Taasisi isiyo ya kiserikali TAREA ilipokabidhi Kompyuta 5 za kisasa aina ya RENOVO (all in one). Kompyuta hizo zilikuwa na vifaa vyake muhimu kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano ya mtandao wa internet, vifaa hivyo ni kama vile wireless adapters na moderm ya internet. Pamoja na vifaa hivyo taasisi hiyo ilikabidhi printa na feni kwa ajili ya matumizi ya kituo hicho cha Walimu. Wakati anamkaribisha mgeni rasmi katika ghafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bw. Marcelin Ndimbwa alitoa shukurani zake kwa taasisi ya TAREA kwa ufadhili huo. Aidha Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi Bw. Lameck Lusesa naye hakusita kutoa shukurani zake za dhati kwa taasisi ya TAREA kwa msaada mkubwa kwa kituo cha walimu Malinyi. Pia Katibu Tawala aliwaomba wahisani hao kuendelea kutusaidia katika maeneo mengine ya wilaya ya Malinyi na isiwe Malinyi pekee kwa wilaya ni kubwa na kote huko pembezoni walimu wanahitaji huduma kama hizo. TAREA pamoja na kuleta vifaa hivyo walianza kwa kukarabati na kuweka mfumo wa umeme jua katika chumba maalum kilichotengwa kwa ajili ya kuzisimika kompyuta hizo. Kwa upande wake mwakilishi wa taasisi hiyo aliposimama aliwashukuru viongozi wa halmashauri ya Malinyi kwa ushirikiano wao waliotoa katika utekelezaji wa mradi huo. Aidha aliwaomba walimu watakaotumia vifaa katika chumba hicho kuwa wazitunze vyema kompyuta na vifaa vyake ili zidumu kwa muda mrefu. Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Malinyi Bw. Sylvester Kalagila na Afisa Taaluma wa wilaya ya Malinyi Bw. Fileteus Nombo waliishukuru sana taasisi ya TAREA kwa msaada huo wa kompyuta na walieleza kuwa taasisi hiyo pia imetoa msaada wa madawati 54 kwa shule tatu za Malinyi, Nawigo na Makugira. Pia wamefunga mfumo wa umeme jua katika shule za sekondari za Malinyi na Kipingo.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.