Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe, Sebastian Waryuba leo amefanya Mkutano na Wananchi wa Kijiji cha makerere Wilayani Malinyi ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.
Katika ziara hiyo Mhe Waryuba amewataka Wananchi wa Makerere kuendelea kufanya kazi na shughuli nyingine za kiuchumi kwa bidii ili uchumi wa Malinyi uendelee kuimarika, na katika kuunga mkono juhudi za maendeleo kijijini hapo Mhe. Mkuu wa Wilaya ametoa ahadi ya mifuko 10 ya saruji ambayo itatumika katika kuendeleza ujenzi wa ofisi za kijiji cha Makerere.
Dc Waryuba pia amewataka Wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kujikita katika kilimo cha kisasa, chenye tija na chenye matokeo makubwa zaidi na katika kufanikisha hilo Wilaya ya Malinyi imejipanga kutoa mbegu za ufuta mweupe kwa Wakulima ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo kwa msimu ujao, Mkuu huyo wa Wilaya pia amewataka Wananchi wa Malinyi kutumia skimu ya umwagiliaji ya Itete kwani Serikali imetoa fedha za kuimarisha skimu hiyo na kuongeza kuwa hakuna anayezuiwa kulima katika skimu hiyo.
Akizungumzia upande wa mifugo, DC Waryuba amesema kwasasa hakuna sababu ya kuwa na mifugo mingi kwasababu maeneo yamekua madogo na hivyo amewataka Wafugaji kubadili matumizi ya mifugo ili kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo, kufuatia hali hiyo Wilaya ya Malinyi inatarajia kuanzisha mazizi ya mifugo katika kata ya Ngoheranga, Kata ya Malinyi, na kata ya Mtimbira ambayo yatatumika kuhifadhia mifugo.
"Sitaki migogoro ya Wakulima na Wafugaji iendelee kushamiri Malinyi, nataka kuitokomeza na hii itawezekana ikiwa mtakubali kubadilika, Mfugaji fuga usimchokoze Mkulima na Mkukima lima usimchokoze mfugaji, Wote tunahitajiana" amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Mhe. Sebastian Waryuba pia ametoa Wito kwa Wafugaji kujiunga katika vikundi vidogovidogo ili kuunda Viwanda vidogovidogo vya ndani vitakavyozalisha nyama na maziwa.
Aidha, DC Waryuba amesema kuwa Wilaya inatarajia kuandaa kongamano la kilimo na ufugaji bora Malinyi na hivyo kuwataka Wakulima na Wafugaji kujitokeza kwa wingi pindi kongamano hilo litakapoanza ili kujifunza namna bora ya kulima na ufugaji,
Akizungumzia kuhusu Mfumo wa Stakabadhi ghalani, DC Waryuba amesema kuwa stakabadhu ghalani ni mwendo mdundo,Wananchi wataendelea kuelimishwa na wataelewa vizuri, na mfumo huo utaendelea kutumika katika mazao ya kimkakati ikiwa ni pamoja na ufuta, korosho,mbaazi, na kunde .
Kwa upande wa zao la Pamba, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa masharti kwa Wanunuzi wote wa pamba Wilayani Malinyi kuwa wapokwenda kwa Wakulima kununua pamba hawataruhusiwa kuchukua pamba hiyo mpaka wailipie.
DC Waryuba pia amewataka Wafanyabiashara Wilayani Malinyi kuunda umoja wa Wafanyabiashara na kutengeneza kampuni ya kuingia kwenye masoko ya kiushindani.
Hata hivyo DC Waryuba amewatahadharisha Wananchi juu ya utabiri wa hali ya hewa ambao unaonyesha kuwa mwaka huu mvua zitanyesha juu ya wastani (Elinino) na hivyo kuwataka Wananchi kwa kushirikiana na TARURA kuchukua tahadhari mapema kwa kuzibua mitaro ya maji ambayo imeziba ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.