Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Malinyi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasgauri ya Wilaya ya Malinyi Ndugu Khamis Jaaphar Katimba amevishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano mkubwa wanaompatia katika kipindi hiki ambacho Nchi inaelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuongeza kuwa ushirikiano huo umemwezesha kutekeleza majukumu yake kama Msimamizi wa Uchaguzi kwa ufanisi.
Ndugu Katimba ameyasema hayo Otoba 5, 2024 katika Kikao cha nne baina yake na Vyama vya siasa Wilayani Malinyi, kikao hicho pamoja na vikao vingine vitatu vilivyotabgulia vimefanyika kwa lengo la kutathimini zoezi la uandikishaji na utekeleazaji wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, ili kuhakikisha Malinyi inabaki kuwa salama kuanzia mwanzo wa uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Uchaguzi utapita lakini Wanamalinyi tutabaki,hatuna sababu ya kuwa na vurugu kwa sababu ya uchaguzi, hatuna sababu ya kuwa na uchaguzi utakaotuachia uhasama miongoni mwetu, sisi tunatakiwa tuungane , tuwe kitu kimoja tuendeleze maendeleo” amesema Katimba
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka uchaguzi ulio imara na uendeshwe kwa kuzingatia 4r zake na mimi kama Msimamizi wa Uchaguzi nazingatia 4r ndiyo maana nimekua nikijibu na kutekeleza kwa haraka na kwa wakati”amesema Katimba
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo kuwa uchaguzi uwe wa haki kwa kuzingatia 4r, Pia amewashukuru viongozi wa vyama vya siasa kwa kushirikiana na Msimamizi wa uchaguzi
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya rufaa ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya Bi Saida Mhanga amewahakikishia Viongozi wa vyama vya siasa kuwa atazingatia haki katika rufaa zote na mapingamizi yatakayowasilishwa katika kamati yake.
Sambamba na hilo Bi Saida Mhanga pia amewaomba Viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia kanuni na miongozo ya uchaguzi wakati wa pingamizi kwa kuwa maamuzi yatakayotolewa na kamati yake yatazingatia miongozo hiyo.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA Wilaya Ndugu Joseph Mwanja amemshukuru Msimamizi wa Uchaguzi kwa
ushirikiano na kutenda haki kuanzia katika zoezi la uandikishaji mpaka wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi Novemba 27, 2024.
Naye katibu wa CUF Wilaya Ndugu Miraji Ngapulila amesema matarajio yake ni kuona hali ya utulivu na uadilifu ikiendelea kuwepo mpaka mwisho wa uchaguzi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa ACT Wilaya Ndugu Abdu Swedi amesema Serikali ina nia njema katika uchaguzi huu hivyo wasitokee watu wachache katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wasio waadilifu kuharibu nia njema ya ufanyikajji Uchaguzi huu kwa kuzingatia 4r za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.