Viongozi na wadau mbalimbali wilayani malinyi mkoani morogoro wametakiwa kuongeza juhudi katika kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi badala ya kuitumia mahakama kama njia pekee ya kupata haki.
Akizungumza katika maadhimisho ya wiki ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya mahakama vilivyopo katika kijiji cha nawigo wilayani hapa, mwakilishi wa mkuu wa wilaya Bi Rehema Rajabu amesema uendeshaji wa kesi mahakamani hutumia muda mrefu pamoja na rasilimali fedha hivyo kuchangia kudumaa kwa maendeleo ya watu.
Bi Rajabu amesema ili kuwe na uchumi imara wa mtu mmoja mmoja, wilaya mkoa na taifa kwa ujumla ni muhimu kuwe na utatuzi wa migogoro kwa njia usuluhishi ambayo ni rahisi, haina gharama na inaokoa muda hali itayopelekea kurejea kwa amani miongoni mwa wanajamii na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha Bi Rajabu ameitaja migogoro ya umiliki wa ardhi, mirathi pamoja na migogoro ya wanandoa kuwa ndio migogoro mikubwa inayojitokeza mara nyingi katika maeneo mengi wilaya hapa na hivyo kutoa rai kwa wananchi kutafakari kwa kina suala utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhisi kabla ya kufikiria kwenda mahakamani.
Kwa upande wake hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya Bwana Samweli Obasi amesema utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ni takwa la kikatiba ambalo utekelezaji wake ni muhimu kwa kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi hapa nchini.
Katika hatua nyingine Bwana Obasi amesema utatuzi wa migogoro nje ya mahakama imekuwa ni namna mbadala ya chombo kikuu cha kuifikia haki kwa wakati na kuendeleza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa kutoa wasaa kwa watu kutekeleza shughuli zao za kujiongezea kipato jambo ambalo huipa serikali mapato na uchumi wa nchi kukua.
Kuadhimishwa kwa wiki ya sheria kunafungua mwaka mpya wa kazi za mahakama kote nchini.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.