Mkuu wa wilaya ya malinyi mkoani Morogoro Mh. Sebastian Waryuba amewataka watumishi wote wilayani hapa kuongeza ari, bidii na ushirikiano katika kazi ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Mh. Waryuba ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa kada mbalimbali wilayani hapa muda mfupi mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uwekaji saini nyaraka za makabidhiano ya ofisi kutoka kwa mtangulizi wake aliyekua mkuu wa wilaya hiyo Mh. Mathayo Maselle, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ulioko katika kijiji cha misegese wilayani hapa.
Mh.Waryuba amesema wilaya ya malinyi ina changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji ushirikiano pamoja na kujitoa kwa kila mtumishi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ili kuweza kujikabili na kuzitatua changamoto kwa ustawi maendeleo ya wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha Mh. Waryuba amewataka viongozi na watumishi waliohudhuria hafla hayo kwenda kuwahamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kujiongezea kipato sambamba na kujiletea maendeleo binafsi badala ya kuisubiri serikali iwafanyie kila jambo.
Pamoja hayo Mh. Waryuba amesisitiza kuwa hatojishughulisha kwa mwananchi atakaelalamikia njaa kutokana na uzembe wake wa kutojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo kwa kuwa ardhi ya malinyi imejaaliwa rutuba nyingi na ni rafiki kwa mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
Kwa upande wake Mh. Mathayo Maselle ( mkuu wa wilaya mstaafu) ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwaaga wananchi, watumishi na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi chote alichokuwa madarakani na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo kwa mkuu kwa mkuu mpya wa wilaya Mh. Waryuba ili wilaya ya malinyi iweze kusonga mbele.
Aidha Mh Maselle amewaomba radhi wale wote aliowakosea katika kipindi chote alichokuwa akihudumu kama mkuu wa wilaya na kuongeza kuwa yeye ni binadamu kama walivyo binadam wengine na pengine alifanya hivyo katika kuhakikisha anayatekeleza vyema majukumu katika kuwaletea maendeleo wananchi kama alivyoaminiwa na Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani.
Mnamo Januari 25 mwaka 2023, Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya nchini ambapo alifanya uteuzi wa wakuu wa wakuu wa wilaya wapya 37, kuwahamisha vituo vya kazi wakuu wa wilaya 48 huku wengine 55 wakisalia katika vituo vyao vya awali.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.