“Natoa maagizo kwa Watendaji wa Kata kuhakikisha kila Kata inakuwa na Kamati ya Usalama ya Kata”
Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dr. Mussa Ally Mussa katika kikao kazi cha kuzungumza, kusikiliza, kutatua kero na malalamiko ya Watumishi kilichowahusisha Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, na Maafisa Tarafa kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.
Dr. Mussa Ally Mussa ameeleza kuwa Kamati hiyo ya usalama ya Kata itaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Mtendaji wa Kata, na Katibu wa Kamati ambaye ni Polisi Kata na Wajumbe wa Kamati hiyo ni Wenyeviti wa Vijiji/Mtaa.
Pamoja na mambo mengine Kamati hiyo itakua na jukumu la kuitisha vikao, kujadili changamoto zilizokuwemo ndani ya Kata na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo pamoja na kutoa taarifa kwa Maafisa Tarafa na Ofisi ya Mkurugenzi.
Aidha, RAS amewataka Watendaji hao kuishi katika maeneo yao ya kazi waliyopangiwa kwakuwa kanuni ya utumishi inasema hivyo lakini pia waweze kupatikana kwa urahisi pale ambapo Wananchi wanaowatumikia wanapowahitaji kwaajili ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
Dr. Mussa Ally Mussa pia amewaelekeza Watendaji kutumia muda wao mwingi kuwahudumia Wananchi na wanapohitajika wapatikane na kuongeza kuwa kutokutumia muda mwingi kwa Wananchi na kutokupatikana pale wanapohitajika kunarudisha nyuma jitihada za utoaji wa huduma kwa Wananchi.
Sambamba na hilo RAS amewataka Watendaji kuyajua vizuri maeneo yao ya kazi kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi wa eneo husika.
Katika hatua nyingine , Dr. Mussa amesema Watendaji wa Vijiji, Kata na Maafisa Tarafa wanatakiwa kuwa karibu na miradi mbali mbali inayoendelea katika maeneo yao ili kusaidia kujua kama kuna wizi au kusuasua kwa miradi hiyo.
“Watendaji ndio wakusanyaji wa mapato ya halmashauri, hivyo tujitahidi katika ukusanyaji wa mapato na baada ya kukusanya tuhakikishe tunazipeleka fedha hizo benki” amesema Dr. Mussa.
Mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi, RAS ametembelea na kukagua mradi wa BOOST katika shule ya msingi Mwembeni mradi umbao umekamilika na mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekodari Kiswago kupitia (SEQUIP) ambao ujenzi wake bado unaendelea.
Akimshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro kwa kufanya kikao kazi cha kuzungumza, kusikiliza, kutatua kero na malalamiko ya Watenda wa Vijiji, Kata na Maafisa Tarafa katika Wilaya ya Malinyi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi Rehema Said Bwasi ametoa wito kwa Watendaji kuyafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa maelekezo yote yaliyotolewa na RAS ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia Wananchi wa Wilaya ya Malinyi.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.