Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kwa kushirikiana na Mamlaka ya mapato TRA Wilayani Malinyi zimetoa elimu ya ukusanyaji kodi ya zuio kwa Wasimamizi wa miradi ya Elimu, Afya,Idara ya fedha na Kitengo cha manunuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.
Mafunzo hayo yaliyotolewa katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri yamelenga kuwajengea uwezo walengwa juu ya namna bora ya ukusanyaji wa kodi ya zuio (Withholding Tax) ili iweze kusaidia Serikali katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa Wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa lengo la kuwaletea Wananchi huduma za kijamii kama vile maji, umeme, barabara afya na elimu.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Malimyi Bi Sikujua Kimweri amesema taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa kodi ya zuio kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi imekuwa haikusanywi kama inavyotakiwa kutokana na kutokua na mwingiliano wa kiutendaji/ kimifumo kunakoziwezesha Ofisi za Halmashauri kusomana hasa pale fedha zinapotolewa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali hali ambayo inapelekea kukosekana kwa takwimu sahihi kwa kipindi tarajiwa.
"kwa manunuzi ya bidhaa na huduma yanayofanyika katika ngazi ya Kata na Vijiji kumekuwa na uelewa mdogo wa uwasilishaji wa kodi hii, Pia zipo taarifa za kuwepo kwa Wafanyabiashara wasiotoa stakabadhi za EFD, changamoto hizi zote zimepelekea mapato haya ya kodi ya zuio kuwasilishwa kwa kuchelewa au kutokukatwa kabisa" amesema Bi Sikujua Kimweri.
Naye Kaimu maneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kituo cha kodi Wilaya ya Malinyi Ndugu John Magembe amesema kuwa kodi ya zuio hukatwa kwenye bidhaa na huduma mbalimbali zinazopatikana au kutolewa katika Halmashauri na kuongeza kuwa aina hii ya kodi hukatwa aslimia mbili 2% kwa manunuzi ya bidhaa yaliyofanyika na asilimia 5% kwa manunuzi ya huduma iliyotolewa.Sheria ya kodi ya zuio imeelekeza kodi hii kukusanywa na mlipaji (Halmashauri) hivyo basi Halmashauri imepewa wajibu wa kuikata kodi hii kutoka kwa watoa huduma na wanaowauzia bidhaa kwa kipindi husika.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.