Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amefanya ziara ya kutembelea miradi pamoja na kukutana na Wananchi wa Vijiji vya Sofi Majiji na Kiswago.
Akiwa katika Kijiji cha Sofi Majiji DC Waryuba ametembelea mradi wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Sofi, Shule ya Msingi Igubika na Shule ya Msingi Majiji ambapo amewasisitiza Wanakijiji kuhudhuria katika Mikutano ya hadhara kwa lengo la kujua mapato na matumizi ya Kijiji na kuongeza kuwa Mikutano ni njia mojawapo ya kubadilishana mawazo baina ya Viongozi na Wanakijiji.
Aidha, DC Waryuba amewataka Viongozi wa Vijiji kuhakikisha kuwa Vijiji vina mpango bora wa Matumizi bora ya ardhi na Wananchi waelimishwe kuwa migogoro ya Wafugaji na Wakulima haifai.
Kwa Upande mwingine Mkuu wa Wilaya huyo amekemea nyimbo au sherehe hasa kwa nyakati za usiku kwani huchangia katika mmomonyoko wa maadili, hupelekea vitendo visivyofaa Kama vile ubakaji, unyanyasaji na kupelekea mimba za utotoni.
Akiwa katika Kijiji cha Kiswago DC Waryuba ametembelea mradi wa Shule ya Msingi Kiswago, na Zahanati ya Kiswago na alipozungumza na Wananchi alisisitiza pembejeo za kilimo hususan madawa yapatikane mapema ili kulinda mazao yasiharibiwe.
Mhe. Mkuu wa Wilaya pia amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kufanya ufuatiliaji wa ujenzi wa soko la Kijiji cha Kiswago baada ya Wananchi kudai kuwa ujenzi wa soko hilo unaenda kwa taratibu sana.
Hata hivyo DC Waryuba amewasisitiza Viongozi wa Wilaya ya Malinyi kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana katika Vijiji vyote bila ya upendeleo.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.