Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amewataka Maafisa ugani kilimo kuimarisha elimu, kutembelea mashamba, kutatua changamoto na kuwashauri Wakulima namna Bora ya kuongeza uzalishaji wa zao la ufuta na mazao mengine.
DC Waryuba ameyasema hayo wakati akizungumza na Wakulima waliokua wakishuhudia Mnada wa zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani uliofanyika kwa njia ya mtandao Julai 14 2023 Wilayani Malinyi.
DC Waryuba amesema kuwa kwa msimu ujao wa kilimo Wilaya ya Malinyi inakusudia kuleta mbegu ya ufuta mweupe ambayo Ina soko kubwa kibiashara, hivyo ni lazima Maafisa ugani kilimo watoe elimu ya kutosha kwa Wakulima, waanzishe mashamba darasa na ufanyike utafiti ili kujiridhisha Kama ufuta mweupe unafaa katika ardhi ya Malinyi.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa Stakabadhi ghalani DC Waryuba amesema kuwa mfumo huo ulianzishwa na Serikali kwa lengo jema la kumuinua Mkulima na akawashauri Wakulima walioshudia Mnada wakawe mabalozi kwa Wakulima wenzao ili wapeleke ufuta Ghalani kwa wingi kuwezesha Mnada unaofuata kufanyika kwa haraka zaidi.
Naye Afisa Kilimo wa Wilaya ndugu Martin muhode akawashauri wanakijiji wa Kijiji Cha Kilosampepo kusajili chama Cha ushirika kwa kuwa lengo la vyama vya ushirika ni kuwawezesha Wakulima kuuza Mazao yao kwa pamoja na kwa manufaa.
Aidha, Afisa Kilimo huyo akaongeza kuwa mara baada ya Mnada kumalizika na Wakulima kuridhia bei kwa pamoja malipo kwa Wakulima yanatakiwa kufanyika ndani ya masaa 72 bila ya kuhusisha tozo ya aina yoyote.
Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya Wakulima wenzake ndugu Yasin Lyandu amesema sasa ana uelewa wa kutosha juu ya mfumo wa Stakabadhi ghalani na yuko teyari kuwashauri Wakulima wengine kupeleka ufuta Ghalani kwa wingi ili waweze kuuza kwa soko la pamoja na kwa manufaa zaidi
Akihitimisha Mnada huo, Afisa Ushirika wa Wilaya ndugu Maliki Mabuba amesema Mnada ujao unatarajiwa kufanyika Malinyi mjini na hivyo Wakulima wapeleke ufuta Ghalani kwa wingi zaidi na wajitokeze kwa wingi siku ya Mnada
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.