Oktoba 6, 2023 Kamati ya Ufundi na Miradi kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira RUWASA Makao Makuu imefanya ziara ya kutembelea Miradi ya Maji iliyopo Wilayani Malinyi.
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ngoheranga mara baada ya kutembelea mradi wa maji uliopo kijijini hapo Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi na Miradi Bodi ya RUWASA Mhandisi Ngwisa Mpembe ameilekeza Ofisi ya RUWASA Wilaya kwa kushikiana na RUWASA Mkoa kusogeza mabomba jirani na makazi ya Wananchi ili Wananchi wavute maji kwa urahisi kwenye Majumba yao.
Aidha Mhandisi Mpembe ameiomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi kuratibu kwa makubaliano na Wanakijiji mahali ambapo patajengwa ofisi ya mradi kati ya Kijiji cha Ngoheranga na Tanga na kuongeza kuwa eneo hilo litakalotumika kwa ujenzi wa Ofisi ya Mradi litumike pia kwa ujenzi wa choo darasa ili Wananchi waweze kujifunza namna gani ya kujenga choo bora kwani kwani jukumu la RUWASA siyo tu kujenga miradi ya Maji bali pia kutoa elimu juu ya Usafi wa Mazingira.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Bodi Ya RUWASA Mhandisi Advera Mwijage amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha akina Mama na familia kwa ujumla wanapata maji safi na salama hivyo akawahimiza Wanakijiji wa Kijiji cha Ngoheranga kutunza vyanzo vya maji ili miradi hiyo ya maji iwe endelevu.
Akitoa elimu kwa Wanakijiji ambao wamedai kuwa ghama za maji ziko juu uniti 1(ndoo 50) kwa shilingi 1600 Meneja Uhusiano na Masoko ndugu Othman Shariff amefafanua kuwa gharama hizo ni za watani na lengo lake ni kusimamia miradi hiyo ili iwe endelevu.
Taarifa iliyosomwa na Meneja wa RUWASA Wilaya Ndugu Chogero Marco imeeleza kuwa mradi wa Ngoheranga ulioanza kujengwa Januari, 2023 na kukamilika Juni 2023 ulijengwa kwa shilingi 641,614,596 na ulilenga kuhudumia Wakazi 10,996 wa Vijiji vya Tanga na Ngoheranga wenye mahitaji ya maji 329.9 mita za ujazo.
Uwepo wa Mradi huo umepelekea kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ngoheranga iliyo jirani na mradi huo ambapo hapo awali Wanafunzi hao walilazimika kukatisha vipindi vya masomo darasani ili kwenda kutafuta maji lakini kukamilika kwa mradi huo kumepelekea kutokukatisha vipindi na hivyo kutumia muda wao mwingi katika masomo hali ambayo imechangia kuongezeka kwa ufaulu wa Wanafunzi katika masomo yao.
Akizungumzia miradi ya Itete Njiwa, Misegese na Igawa ambayo bado haijakamilika Kaim Meneja RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Shaban Daud ametaja sababu zilizopelekea Wakandarasi kutokukamilisha miradi hiyo kwa wakati kuwa ni pamoja na kutokua na Wataalam wa kutosha na uwezo mdogo wa kifedha hali iliyopelekea ujenzi wa miradi hiyo kusuasua kwa muda mrefu na hivyo kuvunjwa kwa mikataba ya Wakandarasi hao, Kufuatia hali hiyo Miradi ya maji Itete Njiwa, Misegese na Igawa itajengwa kwa kutumia Wataalam wa ndani na inatarajiwa kukamilika Januari 2024.
Hata Hivyo, Mwenyekiti wa CCM Tawi la Igawa Ndugu Belton Yonas kwa niaba ya Wanakiji wa Kijiji cha Igawa ameiomba RUWASA kukamilisha mradi huo ndani ya miezi mitatu kama ilivyoahidiwa ili Wanakijiji waondokane na adha ya Maji kijijini hapo.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.