Usaili wa kupata Timu bora za Watumishi katika mchezo wa football na Netball umeanza Oktoba 3, 2023 katika viwanja vya Shule ya Msingi Nawigo na unatarajiwa kumalizika
Oktoba 4, 2023.
Akizungumza na Watumishi wanaoshiriki katika usaili huo Afisa Utumishi Wilaya ya Malinyi Ndugu Tumaini Orotha amewataka Watumishi hao kuonyesha uwezo ili kupata Timu bora itakayowawakilisha Watumishi wote katika mashindano ya Shirikisho la michezo Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) yanayotarajiwa kufanyika Jijini Dodoma Oktoba 18-31/2023.
"Tunafanya jambo muhimu kama Watumishi,tunataka kupata Timu bora ya kuweza kuleta ushindani,Timu hiyo hatuwezi kuipata kwa masihara,tunachokiangalia hapa ni umakini wa kila mmoja wetu"Amesema Ndugu Orotha.
"Manung'uniko hatuyataki,jambo muhimu ni kuonyesha uwezo,akina dada pia tunataka kuondoa hiyo dhana ya kutokushirikishwa,tunataka kuwashirikisha ili na nyinyi mpate Timu bora"Amesema Afisa Utumishi huyo.
Naye Afisa Michezo wa Wilaya Bi Rose Gallus ameeleza kuwa Wachezaji watakaofanikwa kupita katika usaili huo wataendelea na mazoezi kwaajili ya kujiandaa na mashindano ya SHIMISEMITA 2023
Kwa upande wake Kocha wa Timu ya Watumishi Sports Club Ndugu Rashid Muholela amesema kuwa lengo la Viongozi wa Timu hiyo ni kufanya vizuri ili kuingia robo fainali na sio kushiriki mashindano hayo.
Aidha,Kaptein wa Timu hiyo Ndugu Petro Kisiga ameweka bayana kuwa mwaka jana 2022 Timu hiyo haikuweza kufanya vizuri kwa kuwa hakukuwa na maandalizi lakini amefurahi kuona mwaka huu Wilaya imetambua umuhimu wa michezo kwa Watumishi na kuongeza kuwa mwitikio umekua mkubwa kwani Watumishi wengi bora wamejitokeza hivyo anaamini wakaopita katika usaili huo wataunda kikosi imara kitachofanya vizuri katika mashindano hayo.
Hata hivyo,Viongozi wa Timu hiyo wameomba washiriki ambao hawatapita katika usaili huo kutoa ushirikiano kwa kikosi kitachochaguliwa, Viongozi hao pia wamewaomba Wadau mbalimbali wa michezo kujitokeza ili kuisadia Timu hiyo kwa kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.