Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi leo Oktoba 30 imejumuika pamoja na Watanzania wengine na Dunia kwa ujumla katika maadhimisho siku ya Lishe na uzinduzi wa Kampeni ya lishe kwa Vijana balehe ambayo yamefanyika katika shule ya msingi Mchangani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu "Lishe Bora kwa Vijana Balehe, Chachu ya Mafanikio Yao”
Mratibu wa lishe Wilaya ya Malinyi Bi Betrida Makuvila amesema kuwa Vijana balehe(umri wa miaka 10-15) nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za lishe ikiwemo utapiamlo wa aina mbalimbali hususani uzito pungufu, upungufu wa vitamini na madini, uzito au unene uliopitiliza. Udumavu, na ukondefu,
Mratibu huyo wa lishe amefafanua kuwa matokeo ya tathmini ya Malaria na hali ya Lishe kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 10 hadi 15 (School Malaria and Nutrition Survey, 2019) inaonyesha kuwa takriban 6.2% ya wanafunzi hao ni wanene kupita kiasi, 11.2% ni wakondefu, Pia utafiti ulibainisha kuwa watoto wenye umri wa miaka 5-9 na vijana balehe wenye umri wa miaka 10-15 wanakabiliwa na upungufu wa damu, na 42% kuwa na kiwango cha chini cha kushughulisha mwili au kutofanya mazoezi (tabia bwete). Hali ambayo inaathiri ustawi wa kimwili na utendaji wa kiakili wa vijana kwani huhatarisha ufaulu wa mitihani shuleni, hupunguza tija katika uzalishaji mali wanapokuwa watu wazima, na huathiri afya ya uzazi ya sasa na ya baadaye
Aidha, Maadhimisho hayo yameenda sambamba na uchangiaji wa damu salama, upimaji wa VVU pamoja na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto wenye umri wa miaka 10 -15 na utoaji elimu na hamasa katika jamii kuhusu masuala ya lishe kwa akina Mama Wajawazito na wenye watoto chini ya umri wa miaka 5 na vijana balehe ambapo Muhudumu wa Afya ngazi ya Jamii Bwana Kassim Ndyangile ameshauri Vijana na Wazazi juu ya umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kuzingatia mlo kamili unaojumuisha makundi muhimu ya vyakula ambayo ni vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi,vyakula vya asili ya wanyama, mikunde,matunnda, mbogamboga, mafuta, chumvi na sukari kwa kiasi kidogo
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mchangani Bwana Juma Mohamed amewaomba Wazazi washirikiane kuwafundisha watoto umuhimu wa lishe kwa vitendo na kuwaomba Watoa huduma za afya ngazi ya jamii kuhakisha kuwa elimu juu ya lishe inakua endelevu ili watoto wawe na afya bora na wafanye vizuri katika masomo yao.
Maadhimisho ya siku ya Lishe kitaifa yamefanyika katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.