Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba ameungana na Wananchi wa Kata ya Njiwa kuadhimisha siku ya Usafishaji Dunian ambayo katika ngazi ya Wilaya maadhimisho hayo yamefanyika katika Kata ya Njiwa.
Siku hii huadhimishwa kila ifikapo tarehe 16.9.na kwa mara ya kwanza iliadhimishwa Duniani 2019 ambapo Tanzania imeadhimisha siku hii kwa mara ya kwanza mwaka 2022.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo, DC Waryuba amewataka Wananchi kuzingatia suala la Usafi kwenye maeneo ya soko, maeneo yenye mikusanyiko mikubwa, mikusanyiko midogo na mtu mmojammoja kwa kuwa Usafi ni suala muhimu kwa maendeleo ya Afya zetu
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameielekeza Halmashauri ya Wilaya kuhakikisha kuwa katika Kila Kijiji kuwe na kanuni/Sheria ndogondogo za kudhibiti usafi wa Mazingira ili suala la Usafi lipewa kipaumbele.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Afisa Mazingira wa Wilaya Bi Christina Chacha amesema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya 2022 Kata ya Njiwa ina jumla ya Kaya 3788, kati ya Kaya hizo Kaya 3602 ndizo Kaya zenye vyoo ambayo ni sawa na 95% na Kaya 1750 tu ndizo Kaya zenye mashimo ya kuhifadhia taka ambayo ni sawa na 46%, hali ambayo inapelekea Kata ya Njiwa kuwa na muonekano usio nadhifu kutokana na kuzagaa kwa taka katika maeneo mengi yanayozunguka Kata hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Bi Christina Chacha amesema kuwa mikakati ya Halmashauri katika kukabiliana na changamoto hiyo ya Usafi katika Kata ya Njiwa ni kuendelea kutoa Elimu ya usimamizi wa taka na Usafi wa Mazingira kwa kufuata Sheria kanuni na taratibu kwa kushirikiana na Uongozi wa Kata na Vijiji
Naye Afisa Afya wa Wilaya Bwana Benard Mbumbumbu amewataka Wafanyabiashara kuhakikisha kuwa Wana mifuko/ vifaa vya kuhifadhia taka katika maeneo yao ya biashara na Uongozi wa Vijiji uandae utaratibu wa kuchukua taka hizo na kuzipeleka eneo maalum la kutupia taka .
Aidha, Afisa Afya huyo pia amewataka Wananchi wa Kata ya Njiwa kujenga vyoo bora na vya kudumu ili kulinda na kuimarisha Afya zao na pia waweze kunufaika na fursa ya Lipa kwa Matokea inayolenga kuwatambua Wakuu wa Kaya wenye vyoo bora na vya kudumu.
KAULI MBIU: Tuungane Pamoja Kujifunza, Kupanga na Kuhimiza Uimarishaji Huduma za Uhifadhi Taka.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.