Wanawake wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro leo Machi 8, 2024 wameungana na wanawake wengine Nchini kusherehekea siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka .
Maadhimisho hayo ambayo kiwilaya yamefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nawigo yalianza kwa maandamano ambayo yalihusisha Wanawake kutoka kada mbalimbali wakiwemo Wanawake wajasiriamali yalipokelewa katika viwanja vya shule ya Msingi Nawigo na Mbunge wa Jimbo la Malinyi Mhe. Antipas Mgungusi ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika. maadhimisho hayo.
Katika maadhimisho hayo Mhe. Mgungusi amepata wasaa wa kusikiliza na kujibu risala ya wanawake ambayo iligusia mambo mbalimbali ikiwemo uwepo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Malinyi, uhitaji wa mabweni ya wanafunzi wa kike kwa shule ambazo ziko mbali na makazi ya watu, athari za mafuriko zilizojitokeza katika shughuli za uzalishaji mali za Wanawake, ubovu wa barabara inayoanzia Ifakara, Malinyi hadi Kilosa Mpepo, Wanawake kupewa kipaumbele katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni pamoja na uhitaji wa elimu ya jinsi ya kuzalisha na kusimamia miradi kwa vikundi vya Wanawake ambao wanapata mikopo kutoka 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Aidha, Mhe. Mgungusi amekabidhi zawadi kwa Wanawake wajasiriamali wenye ulemavu ambao wameonyesha jitihada katika ujasiriamali dhidi ya ulemavu walio nao, kikundi cha ushonaji Misegese ambacho kimefanya vizuri katika marejesho, pamoja na Wanawake walioonyesha jitihada zaidi tangu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Wanawake yalipoanza.
Sambamba na hilo, Mhe. Mgungusi amezindua jukwaa la Wanawake Wilaya ya Malinyi, amechangia uwezeshaji kiuchumi wa jukwaa hilo pamoja na kuhamasisha Wadau mbalinbali waliodhuria maadhimisho hayo kuchangia fedha ili Jukwaa hilo liweze kusimama imara.
Hata hivyo, Mbunge wa Malinyi Mhe. Antipas Mgungusi amekabidhi mahitaji muhimu ya kuanzia kidato cha kwanza ambayo yametolewa na Chama cha Wafanyakazi TALGWU Wilaya ya Malinyi kwa binti ambaye alimaliza dara la saba na kufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini Wazazi wake hawakuwa tayari kumuendeleza binti huyo kimasomo na badala yake Wazazi hao walitaka binti aolewe.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.