Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mhe. Pius Mwelase tarehe 22/8/2023 ameongoza mkutano wa kuwasilisha taarifa za Kata robo ya nne 2022/2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.
Akifungua mkutano huo uliohudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Madiwani, Watendaji wa Kata, Wakuu wa Idara na Vitengo Mhe. Pius Mwelase amesisitiza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi imejipanga kuhakikisha kuwa miradi yote inayokuja Malinyi inatejelezwa kulingana na bajeti iliyotengwa na kukemea utekelezaji wa Miradi kinyume na bajeti iliyokusudiwa
Mhe. Mwenyekiti amewataka Madiwani kila mmoja katika eneo lake kutembelea miradi hiyo ili kujua matumizi sahihi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo kwakuwa wao ndio Wasimamizi wa miradi hiyo na kuongeza kuwa Halmashauri haiko teyari kupata sifa mbaya ya kutokutekeleza miradi kwa wakati.
Pamoja na kupitia, kujadili ajenda za mkutano huo Wageni waalikwa pia walipata nafasi ya kujifunza fursa za kuwekeza katika kilimo cha ufuta mweupe kutoka kwa Watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) kituo cha Naliendele Mtwara ambapo imeelezwa kwamba mbegu za ufuta mweupe zina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuzalisha kwa wingi katika eneo dogo.
Aidha Mhe. Pius Mwelase amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba kwa kuwakaribisha Watafiti hao kutoa Elimu katika mkutano huo ambapo amewataka Madiwani na Maafisa Ugani kilimo Wilaya ya Malinyi kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia Wakulima katika maeneo yao na ameagiza kuanzishwa mashamba darasa ili Wakulima wajifunze kwa vitendo, na wazalishe ufuta wenye soko.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.