Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi. Rehema Bwasi amekiri kupokea mradi wa Lishe endelevu kutoka Shirika lisilo la Kiserikali Save the Children International Julai 14, 2023 katika kikao cha tathimini ya afua za lishe robo ya nne (4) April-June kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Akizungumza katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti DC Sebastian Waryuba na kuhudhuriwa na Wakuu wa Idara mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji amesema Save the Children International wamefanya kazi kubwa sana katika kutekeleza mradi huo na hivyo Wilaya ya Malinyi kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya Kilimo inawajibika kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakua endelevu kwa kuwa suala la lishe bora ni muhimu sana ili kupata jamii yenye Afya Bora
Naye Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba ameisisitiza kamati ya lishe endelevu kupokea, kuumiliki na kuuendeleza mradi huo na akatoa nafasi ya kushauriana, kurekebishana ili mradi huo uweze kusonga mbele na kuhakikisha kizazi chetu kinakua na afya inayostahili.
Akikabidhi mradi huo, Meneja Mradi wa Lishe endelevu Emmanuel Michael amesema kuwa mradi huo wa Lishe endelevu Wilayani Malinyi uliotekelezwa kwa miaka mitano (5) kuanzia 2018-2023 ulilenga kufikia matokeo makuu 3 ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya lishe ambapo Watendaji walijengewa uwezo juu ya masuala mbalimbali ya lishe, kuimarisha Hali ya lishe katika ngazi ya jamii ambapo mradi ulifanya kazi na wahudumu wa afya 59 katika ngazi ya jamii,vituo vya afya 11na kuwajengea uwezo Walimu 27 wa shule za Sekondari, na kuhakikisha upatikanaji na uzalishaji wa chakula chenye virutubisho vya kuondoa udumavu.
Pamoja na makabidhiano ya mradi wa Lishe endelevu,Kamati ya lishe endelevu chini ya Mwenyekiti DC Waryuba pia ilipokea taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kutoka Idara ya Afya, Idara ya Elimu Msingi, Idara ya Elimu Sekondari, Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, Idara ya Mifugo na Uvuvi, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Watoto, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.