Kikao hicho kilifanyika kufuatia barua iliyoandikwa na Wafanyabiashara wa Wilaya ya Malinyi kwa Mkurugenzi juu ya ongezeko la ushuru wa mazao yanayosafirishwa nje ya Wilaya, kutokukubaliana na Mfumo wa Stakabadhi Ghalani pamoja na kutokukubaliana na tozo za Taka.
Wafanyabiashara hao wameeleza kwamba mabadiliko hayo ya tozo pamoja na utekelezaji wa mfumo wa Stakabadhi ghalani umesababisha kushuka kwa mzunguko wa fedha ndani ya Wilaya na kufanya Wafanyabiashara kutoka nje ya Wilaya kutonunua mazao hususan mchele.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi Rehema Bwasi amesema kuwa Halmashauri imepitia na kutathimini tozo za biashara za mazao ya Kilimo na kubaini kuwa tozo hizo za awali ni za muda mrefu na haziendani na bei ya soko ya mazao hayo.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Halmashauri imepitia vyanzo vyake vya ndani vya mapato kwa kutumia Sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa sura ya 290 ya mwaka 2019 ili viendane na bajeti ya sasa 2023/2024 ya bilioni 3.5 inayotokana na vyanzo vya ndani vya mapato.
Mabadiliko hayo ya tozo pia yalifanyika kwa kuzingatia 3% ya bei ya soko ya mazao husika ikiwa na dhamira ya kupata mapato na kuwa na matumizi sahihi ya 40% kwa 60%.
Kuhusu Mfumo wa Stakabadhi Ghalani Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa utekelezaji wa mfumo huo sio utashi wa Mkurugenzi , menejimenti yake na Waheshimiwa Madiwani bali ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo yenye lengo la kumlinda Mkulima.
"Tutafanya kikao cha tathimini juu ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili tujue tumetoka wapi, tumekum ana na changamoto zipi na katika msimu mwingine tufanye Nini ili tuende vizuri zaidi" amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Aidha, kuhusu ushuru wa taka, Bi Rehema Bwasi amefafanua kuwa kinachotekelezwa ni Sheria ndogo za Usafi wa mazingira za Wilaya za mwaka 2017 ambapo biashara ndogo hutozwa shilingi 2000, biashara za kati shilingi 5000 na biashara kubwa shilingi 10000 kwa mwezi kiwango ambacho ni kidogo na hakitoshelezi gharama za ubebaji taka kutoka eneo la biashara mpaka eneo la kutupa taka, Lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza Halmashauri inajipanga kutoa Elimu zaidi na kukutana na Wananchi ili waweze kutoa mapendekezo yao.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi amewasihi Wafanyabiashara kukubaliana na tozo hizo kwani zinalenga kuendeleza Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi na amaahidi kutoa ushirikiano kwa Wafanyabiashara na Wananchi kwa ujumla katika mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.