Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipera Asilia katika Kata ya Njiwa Wilayani Malinyi Ndugu Doto Ng'unda Lala amesimamishwa uongozi wa Kijiji hicho Agust 21, 2023 katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Kijiji Wakulima pamoja na Wafugaji wa Kijiji hicho.
Mhe. Mkuu wa Wilaya amefikia uamuzi huo mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Wanakijiji na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji hicho kuwa Mwenyekiti huyo amekua ni kichocheo cha ukosefu wa maendeleo katika Kijiji hicho.
Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema kuwa Kijiji kimedumaa, Kijiji hakina maendeleo na kuwa amepokea tuhuma nyingi dhidi ya Mwenyekiti huyo sasa Serikali ya awamu ya Sita haiwezi kufanya kazi katika mazingira hayo.
"Kichocheo cha maendeleo ni Kiongozi wa Serikali lakini Kiongozi huyu hana dira, Hana mwelekeo na hivyo Wajumbe wa Serikali ya Kijiji wote wanamlaumu Kiongozi wao "amesema Mhe. Sebastian Waryuba.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Njiwa Ndugu Issa Mateku amethibitisha kuwa matatizo yaliyo katika Kijiji hicho yamesababishwa na Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa licha ya kaitwa na kuonywa katika vikao mbalimbali vya Serikali ya Kijiji lakini Mwenyekiti huyo ameendelea na mienendo yake isiyofaa katika Kijiji hicho.
"Mwenyekiti huyu amekua ni msindikizaji wa matatizo katika Kijiji hiki, Kuna watu wamepigwa na kupasuliwa kwa sababu yake na ni kichocheo cha ukosefu wa maendeleo katika Kijiji hiki" amesema Mwenyekiti wa CCM Kata ya Njiwa
Alipopewa nafasi ya kuzungumza mbele ya hadhara hiyo Mwenyekiti huyo wa Kijiji Ndugu Doto Ng'unda Lala amesema kuwa ana uzoefu mkubwa katika nafasi hiyo, na ameingia kuitumikia Ipera Asilia kwa moyo mmoja pamoja na kukitumikia Chama Cha Mapinduzi na siyo kuleta mgawanyo wa makundi katika Kijiji hicho.
Kufuatia kusimamishwa uongozi kwa Mwenyekiti huyo Mkuu wa Wilaya ameagiza Wajumbe wa Serikali ya kijiji leo Agost 22, 2023 wachague Mwenyekiti wa muda atakayesimamia miradi ya Serikali ya Kijiji wakati utaratibu rasmi wa kisheri wa kumuondoa Ndugu Doto Ng'unda Lala katika uongozi huo ukiendelea.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.