Tasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Wilaya ya Malinyi imefanya kikao kilichowakutanisha wadau wa huduma zitolewazo na idara ya ardhi kama vile Ofisi ya Mwanasheria, Idara ya Ujenzi, Watumishi idara ya ardhi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Malinyi
Akitoa neno la utangulizi katika kikao hiko kilichofanyika Februari 29, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri Kaimu Mkurugenzi Ndugu Gasto Silayo ameishukuru TAKUKURU kwa kuona umuhimu wa kujadili huduma zitolewazo na idara ya ardhi kwakuwa sekta ya ardhi Wilayani Malinyi imekuwa ikikumbwa na changamoto za mara kwa mara ikiwemo migogoro kati ya vijiji na vijiji, migogoro kati ya taasisi za kidini na taasisi za Kiserikali pamoja na migogoro ya wananchi mmoja mmoja.
Aidha katika kikao hiko, Mkuu wa TAKUKURU (W) Bi Sikujua Kimweri ameeleza kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa no.11 ya mwaka 2007 katika kifungu cha 7 kimeipa TAKUKURU majukumu ya kuzuia vitendo vya Rushwa kwa kuchambua mifumo ya utoaji huduma na kuongeza kuwa lengo la kikao hiko ni kujadili namna idara ya ardhi inazingatia sheria, kanuni na taratibu katika utoaji wa huduma za ardhi.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa TAKUKURU (W) ameeleza kuwa TAKUKURU imeonelea ipo haja ya kufanya uchambuzi huo kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za ardhi ikiwemo migogoro ya ardhi, migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo inaikosesha serikali mapato kutokana na kodi mbalimbali kutokukusanywa kwa ufanisi ikiwemo kodi ya zuio na vibali vya ujenzi.
Bi Sikujua Kimweri amezitaja changamoto kadhaa zinazopelekea kuwepo kwa huduma duni za ardhi ikiwa ni pamoja na elimu duni juu ya utolewaji wa vibali vya ujenzi, kuwepo kwa migogoro ya ardhi kunakosababishwa na uwajibikaji hafifu wa watendaji ngazi za vijiji, uhaba wa vitendea kazi na bajeti isiyokidhi mahitaji, uchache wa watumishi idara ya ardhi, uundwaji wa baraza la ardhi na nyumba la wilaya, changamoto ya kutokuwepo kwa maeneo yaliyopimwa na kutengwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2023.
Hata hivyo, Afisa ardhi mteule (W) Ndugu Edward Lugakingira ameeleza kuwa mchakato wa kupata wajumbe wa Baraza la ardhi na nyumba la Wilaya umeshakamilika na sasa maandalizi yanayoendelea ni kumalizia jengo ambalo Baraza hilo litafanyia shughuli zake, jengo hilo linatarajiwa kukamilika ndani ya muda mfupi.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.