Wazazi Jamii ya Wafugaji katika Kijiji Cha Kiswago Kata ya Sofi watakiwa kuwapeleka watoto wa kike shuleni kupata Elimu na kutothubutu kuwaozesha katika umri mdogo kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inajitoa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha watoto wa kike na watoto wa kiume wanapata nafasi sawa katika Elimu.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Malinyi Bi Rehema Rajabu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika mkutano na Wanakiji wa Kata ya Sofi, Maafisa kutoka idara ya Manunuzi, Muhandisi Majengo,Ofisi ya ardhi na Maafisa kutoka Divisheni ya Elimu Sekondari wa kuutambulisha mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kiswago kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wenye thamani ya shilingi 528, 998, 425 .
Aidha, Kaimu Katibu Tawala amewapongeza Wanakijiji na Serikali ya Kijiji cha Kiswago kwa kutoa eneo lenye ukubwa wa ekari 33.5 kwaajili ya ujenzi wa Shule hiyo na kuongeza kuwa ili mradi huo uweze kuwanufaisha wakazi wa Kiswago kipaumbele kitolewe kwa mafundi na wasaidizi wa mafundi ambao ni Wakazi wa Kijiji cha Kiswago kwaajili ya ujenzi huo.
Hata hivyo, Bi Rehema Rajabu amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo ushirikiano wa dhati unahitajika kutoka kwa Wanakijij ili mradi huo ukamilike ndani ya wakati, na akawaomba Wanakijiji wafuatilie mradi huo kwa ukaribu na watoe taarifa kwenye Ofisi ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya pale watakapoona mradi huo umesimama.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Wilaya ya Malinyi Bi Pendo Masalu akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ameweka bayana kuwa Mradi huo unatakiwa kukamilika mapema iwezekanavyo ili itakapofika januari 2024 Wanafunzi waanze kusoma katika Madarasa hayo.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.