Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mheshimiwa Sebastian Waryuba amefungua Kikao cha kuratibu zoezi la kitaifa la ugawaji wa vyandarua kwenye kaya bila ya malipo kwa Wilaya ya Malinyi. Kikao hiko kimefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya tarehe 13 Januari 2026.
Akifungua Kikao hiko Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Sebastian Waryuba amesema Serikali ya Wilaya ipo tayari kuhamasisha Wananchi Vijijini kwani Vyandarua ni njia ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria ambao ni ugonjwa unaosumbua sana Wananchi wa Malinyi ambao idadi yao ni zaidi ya Watu 278,000.
DC Waryuba amesema ni marufuku kwa Wananchi kuviuza vyandarua vitakavyotolewa kwani Serikali inatumia gharama kubwa kugharamia vyandarua lakini vinatumika na Wananchi kwa Uvuvi na wengine wanatumia kwenye kilimo cha Nyanya na Vitunguu hivyo amesisitiza inabidi iundwe Sheria Ndogo ( By Law) kuzuia matumizi hayo.
Kwa upande wa Mratibu wa zoezi la ugawaji wa vyandarua kutoka Wizara ya Afya- Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria Ndugu Peter Gitanya amesema vyandarua vitagawiwa kwa ngazi ya vijiji na vitongoji ambapo kila Watu wawili (2) watapata chandarua kimoja. Na vyandarua hivyo havina madhara yoyote kwa Afya ya Binadamu. Ndugu Peter Gitanya ameomba Watendaji wa Kata na Vijiji waandikishe taarifa sahihi ili kila Kaya Wilayani Malinyi iweze kupata vyandarua bila malipo. Na kaitaka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ( DED) itoe taarifa kila wiki namna zoezi linavyoendelea.
Kwa upande wa Viongozi wa Dini wameahidi kufikisha ujumbe wa zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa Waumini wao. Mapema akiwasilisha Mada ya Uhamasishaji Kampeni ya Ugawaji wa Vyandarua kwenye Kaya bila Malipo Ndugu Gitanya amesema Halmashauri ya Malinyi kwa Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 7 zenye maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Malaria kati ya Halmadhauri 9.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.