Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amewataka Wasimamizi wa mikopo ya Vikundi vya mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu kuwa waaminifu kwenye fedha wanapovisimamia vikundi hivyo.
Mhe. Waruba amesema hayo septemba 26, 2024 alipokuwa akifunga mafunzo ya wasimamizi wa mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Aidha, Mhe. Waryuba amesema kuwa anaamini waliopata mafunzo hayo ya usimamizi wa mikopo wataenda kutenda vyema na fedha zitaenda kuchakatwa vizuri na kusimamia uendeshaji wake bila kuwepo na malalamiko yoyote kwa kuhakikisha mikopo inatolewa kwa vikundi vyenye sifa.
Sambamba na hilo, Mhe. Waryuba amewataka Viongozi wa serikali za mitaa kuwasomea Wanakijiji wao taarifa za mapato na matumizi ya kijiji kabla ya tarehe 20 oktoba, 2024 na kuongeza kuwa taarifa hizo zipelekwe kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na kufikishwa kwake ili kuhakikisha maelekezo hayo yamefanyiwa kazi kwa usahihi.
Pia Mhe. Waryuba ametoa pongezi kwa waaandaaji wa mafunzo hayo na kuwataka wakajitume na kufanya kazi kwa haki ili fedha zilizotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zifanye kazi iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Ndugu Khamis Jaaphary Katimba ambaye pia ndiyo Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Malinyi amesema kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unakaribia hivyo shughuli mbalimbali za uhamasishaji zimekwishaanza kufanyika na hivyo amewaomba Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Wananchi wote kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika na kumalizika kwa usalama.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.