Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amezindua program ya visima 900 vya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika ngazi ya Wilaya.
Uzinduzi huo ambao umefanyika Septemba 13, katika KItongoji cha Kitiliwele Tarafa ya Malinyi ni miongoni mwa visima 5 ambavyo Wilaya ya Malinyi imepatiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika program hiyo ya visima 900.
Katika uzinduzi wa Program hiyo Mhe. Waryuba aliambatana na Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Malinyi ambapo amewataka Wakazi wa Kitongoji hiko na Wilaya nzima ya Malinyi kutunza visima hivyo mara vitakapokamilika ili viweze kuwa endelevu.
Akisoma taarifa ya utekelezaji ya program hiyo Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira RUWASA (W) Ndugu Marco Chogero amesema programu ya visima 900 vya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mradi unaohusisha uchimbaji wa visima na uendelezaji wa ujenzi wa visima maeneo ya Vijijini ambako kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na Salama.
Meneja Chogero ameeleza kuwa kwa Wilaya ya Malinyi program ya visima 900 vya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahusisha utekelezaji wa miradi mipya mitano katika Kijiji vya cha Kiswago Kitongoji cha Salamiti, Kijiji cha Malinyi Kitongoji cha Kitiliwele, Kijiji cha Ihowanja, Kijiji cha Mabanda, na Kijiji cha Kilosa Mpepo
"Katika kutekeleza program hii Wilaya ya Malinyi Serikali imetenga kiasi cha shilingi 300,000,000 ambapo kwa kila mradi zimetengwa shilingi 60,000,000 na kukamilika kwa program hii kutaongeza wigo wa upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Malinyi ambapo watu 5500 sawa na asilimia 2.44% watafaidika na huduma ya maji kupitia program hii" amesema Ndugu Chogero
Hata hivyo akizungumza kwa niaba ya Wakazi wa Kitongoji cha Kitiliwele, Mwenyekiti wa Kitongoji hiko ndugu Lutamla Kujelwa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa mradi huo ambao utasaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa maji safi na salama na kuongeza kuwa Kitongoji hiko bado kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara hasa kipindi cha masika.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.