Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amesema kuwa sasa mashauri na kesi zote za migogoro ya ardhi zimeanza kusikilizwa rasmi kupitia Baraza la ardhi na nyumba Wilayani Malinyi.
Mhe. Waryuba ameyasema hayo leo Machi 24, 2025 wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii mara baada ya huduma ya kusajili na kusikiliza mashauri na kesi za migogoro ya ardhi kuanza rasmi katika Wilaya ya Malinyi.
"Namshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kwa huduma hii Wilayani Malinyi, ujaji wa Baraza la ardhi na nyumba katika Wilaya yetu ni utekelezaji wa 4R za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu Baraza la ardhi la Kata linatoa usuluhishi kupatanisha Wananchi wenye migogoro ya ardhi kabla ya kulumbana na kupelekana Mahakamani,hivyo falsafa hii ya Mhe. Rais ni nzuri sana kwani inaleta Amani na utulivu katika maeneo yetu" amesema Mhe. Waryuba.
Aidha Mhe. Waryuba amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ndugu Khamis Jaaphar Katimba kwa kuwezesha upatikanaji wa Ofisi zitakazotumika kutolea huduma hii ya kusajili na kusikiliza mashauri na kesi za migogoro ya ardhi ambapo kwa sasa huduma hii itapatikana katika jengo la Ofisi ya ardhi lililopo eneo la Misegese.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la ardhi na nyumba Wilaya ya Malinyi ndugu Richard Mmbandu amesema kuwa Baraza hilo limeanza kazi rasmi Wilayani Malinyi hivyo Wakazi wa Wilaya ya Malinyi wenye mashauri na migogoro ya ardhi wanakaribishwa kwenda kusajili na kusikilizwa mashauri yao mara mara baada ya kupita katika hatua ya usuluhishi katika baraza la Kata na kupatiwa cheti cha usuluhishi.
Ndugu Emmanuel Senga na Bi. Esha Rashidi ambao ni Wakazi wa Wilaya ya Malinyi wenye migogoro ya ardhi waliofika katika ofisi za Ardhi Wilaya ya Malinyi kwaajili ya kusajili na kusikilizwa mashauri yao wamemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba na Mkurugenzi Mtendaji Khamis Jaaphar Katimba kwa kuwasogezea huduma hiyo ambapo hapo awali walitumia gharama kubwa na kusafiri umbali mrefu kwenda Wilaya ya Ulanga na Wilaya ya kilombero kwaajili ya kupata huduma hiyo.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.