Wilaya ya Malinyi Oktoba 13, 2024 Imeongoza matembezi ya hisani ya Zaidi ya kilometa 3 kuhamasisha Wananchi wa Wilaya ya Malinyi kujiandikisha katika orodha ya Wapiga kura zoezi ambalo lilianza rasmi Oktoba 11 na litarajiwa kukamilika Oktoba 20, 2024
Matembezi hayo ya hisani yamefanyika katika Tarafa 3 za Wilaya ya Malinyi ambapo Tarafa ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba ameongoza Wananchi katika matembezi hayo, Tarafa ya Mtimbira Katibu Tawala wa Wilaya Bi Saida Mhanga amewaongoza Wananchi, na Tarafa ya Ngoheranga Msimamizi wa Uchaguzi Malinyi Ndugu Khamis Jaaphar Katimba ameongoza Wananchi katika matembezi hayo.
Matembezi ya hisani Malinyi pia yamelenga kuadhimisha kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni pamoja na kuhitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru tukio ambalo limefanyika Oktoba 13, 2024 Jijini Mwanza.
Akizungumza na Washiriki wa matembezi ya hisani katika Tarafa ya Malinyi DC Waryuba amesema kuwa Ili kushiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa sio lazima uwe na kadi au kitambulisho cha mpiga kura, ukiwa na miaka 18 na kuendelea unaruhusiwa kwenda kujiandikisha katika kituo kilicho karibu yako.
DC Waryuba pia amesema kuwa Uchaguzi wa Serikali za mitaa ni Uchaguzi wa Serikali za wenyeji, watu wanaohusika katika eneo hilo, hiyo ni vyema kuhakikisha kuwa wenyeji wote wa Malinyi wanashiriki kikamilifu katika kujiandikisha na kupiga kura .
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi Bi Saida Mhanga amewaomba wakazi wa Tarafa ya Mtimbira na Wilaya nzima ya Malinyi kujijitokeze kujiandikisha ili wawe na sifa ya kuchagua Viongozi wanaowataka kwa maendeleo ya Malinyi.
Aidha Bi saida Mhanga ametoa rai kwa Wananchi wote wa Malinyi wenye umri wa miaka 21 na kuendelea kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Malinyi Ndugu Khamis Jaaphar Katimba amesema kuwa zoezi la matembezi ya hisani limehusisha Vijana kwa kiasi kikubwa ili vijana hao wapeleke ujumbe wa kujiandikisha na kupiga kura kwa Vijana wenzao pamoja na wazazi wao.
Akizungumzia suala la usalama tangu zoezi la uandikishaji lilipozinduliwa rasmi Msimamizi huyo wa uchaguzi ameeleza kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri hakuna dosari kubwa zilizojitokeza na kuongeza kuwa uhamasishaji unaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Malinyi ili kujenga uelewa Zaidi kwa Wananchi.
Hata hivyo, Ndugu Katimba mara baada ya kukamilisha zoezi la matembezi ya hisani katika Tarafa ya Mtimbira amefanya mkutano na vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa Wilayani Malinyi ili kufanya tathimini pamoja ya zoezi la uandikishaji tangu lilipozinduliwa rasmi Oktoba 11, 2024 na kuongeza kuwa Malinyi inatarajia kuandikisha wapiga kura Zaidi ya 100,00.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.