Wahe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi wametakiwa kuwa mfano wa kutoa hamasa kwa Wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 27, 2024 ili Wananchi waweze kujitokeza kwa wingi kuchagua Viongozi wanaowataka na kuhakikisha Uchaguzi unafanyika kwa haki, Amani na utulivu.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi Bi Saida Mhanga wakati akitoa neno la Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba katika baraza la kawaida la Madiwani lililofanyika leo Oktoba 30 kwa ajili ya kujadali taarifa za utekelezaji robo ya kwanza Julai- Septemba katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Bi Saida Mhanga pia amewataka Viongozi na timu ya Wataalamu kutoka Halmashauri kuhakikisha miradi yote Serikali inayotekelezwa Malinyi inatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na kuongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo uendane na thamani ya pesa amabazo Serikali inagharamia ili kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mhe. Pius Mwelase ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngoheranga amewaomba Wahe. Madiwani kusimamia vyanzo vya makusanyo vya mapato katika maeneo yao ili Halmashauri iweze kukusanya kwa Wingi na kukamilisha miradi iliyokusudiwa kutekelezwa kwa mwaka huu 2024/2025.
Aidha Mhe. Mwelase amesema kuwa mara baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kumalizika Halmashauri inatarajia kuendesha semina elekezi kwa Watendaji ngazi ya Vijiji ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Ndugu Khamis Jaaphar Katimba amesema Malinyi inaendelea vizuri ambapo mpaka mwezi kufikia Oktoba 2024 Halmashauri imekusanya kwa asilimia 60, na kuongeza kuwa asilimia 40 ya makusanyo hayo inakwenda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Sambamba na hilo Ndugu Katimba amewashukuru Wajumbe wa Baraza la madiwani kwa kuzingatia mafunzo ya utawala Bora aliyoyatoa mwezi Septemba ambapo mafunzo hayo yamewezesha Mkutano huu wa Baraza la Madiwani kwa mara ya Kwanza kufanyika chini ya dakika 30 na kuwaomba Wajumbe hao ushirikiano Zaidi katika kutekeleza majukumu mengine ya Serikali.
Hata hivyo Mjumbe wa Kamati ya fedha, Uongozi na Mipango ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Itete Mhe. Anatory Libawa amesema Wahe. Madiwani kwa pamoja wamekubaliana kupunguza ushuru wa pumba kutoka sh. 1500 hadi sh 500 ili kutoa nafasi kwa Wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali kuja Malinyi kununua pumba kwa wingi Zaidi.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.