Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amesema kuwa Wananchi wa Wilaya ya Malinyi wanahitaji huduma bora za afya kutoka kwa Wataalam wa afya.
Mhe. Waryuba ameyasema hayo Agost 28, 2024 wakati akizungumza katika kikao cha uwasilishaji wa taarifa za robo ya nne (April-Juni kwa mwaka 2023/2024) kutoka kwa timu ya waendeshaji huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na Wadau wanounga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya afya.
Mhe. Waryuba amesema kuwa huduma zinazotolewa na Wataalam wa afya zinapimwa na Wananchi hivyo amewaomba Wataalam hao kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa Wateja wao kwani utoaji wa huduma bora hauhitaji pesa bali ni moyo wa upendo wa mtoa huduma kwa mteja wake.
“Nawasihi baada ya kikao hiki nendeni mkafanye kazi upya, mnapotoa huduma jaribuni kuvaa viatu vya Wagonjwa, kuweni na mawasiliano mazuri na Wagonjwa na wafanyeni Wagonjwa watamani kurudi tena kupata huduma katika vituo vyenu vya kutolea huduma za afya.” Amesema Mhe. Waryuba
Aidha, Mhe. Waryuba amesema anatambua kuwa sekta ya afya inakabiliwa na uhaba wa Watumishi hivyo amewasihi Wataalam hao wa afya kufanya kazi kwa upendo kwani Serikali bado inaendelea kuajiri Watumishi katika sekta hiyo.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Wilaya ameielekeza Ofisi ya Mkuu wa divisheni ya afya, ustawi wa Jamii na Lishe kuhakikisha kuwa Vijana wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika sekta ya afya wanatekeleza majukumu yao chini ya usimamizi wa Watumishi wazoefu.
Kikao hiko kililenga kupitia na kufanya tathimini ya shughuli za afya zilizofanyika katika robo ya nne 2023/2024 ambapo afua mbalimbali zimewasilishwa na kuonesha sehemu ambazo Halmashauri imefanya vizuri na sehemu ambazo Halmashauri haikufanya vizuri zimewekewa mpango mkakati wa maboresho zikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za dawa na vifaa tiba,huduma za chanjo, kifua kikuu na huduma zote zinazotekelezwa kwa kushirikiana na Wadau
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.