Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilayani Malinyi imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Tarafa ya Malinyi ikiwa ni sehemu ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha CCM Wilayani Malinyi kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2024.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ufungaji wa mashine ya umeme eneo la stendi ya mabasi Misegese, Uzinduzi wa visima 900 vya Mama Samia, Jengo la dharura Hospitali ya Wilaya, Mradi wa ujenzi wa shule ya msingi Misegese, Mradi wa barabara Misegese-Lugala-Kiwale pamoja na mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Malinyi.
Kamati hiyo ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilayani Malinyi imeitaka Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo Wilayani Malinyi inajengwa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika, miradi hiyo ikamilike kwa wakati na mara baada ya kukamilika miradi hiyo itunzwe ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
Aidha Kamati hiyo imepongeza huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Malinyi na imeuelekeza uongozi wa Hospitali hiyo kutangaza huduma mbalimbali zinazotolewa katika Hospitali hiyo ili Wananchi waweze kuzifahamu na kuzitumia.
Ziara ya kamati ya Siasa ya chama cha Mapinduzi Wilayani Malinyi imeanza Septemba 13, 2024 katika Tarafa ya Malinyi, Septemba 14, 2024 Kamati hiyo itakagua miradi ya maendeleo katika Tarafa ya Ngoheranga na Septemba 15, 2024 Kamati hiyo itahihitimisha ziara yake katika Tarafa ya Mtimbira.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi
Postal Address: 18 Malinyi, Morogoro
Telephone: 0643111999
Mobile:
Barua pepe za watumishi: ded@malinyidc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.